Wednesday, September 15, 2010

KIKWETE UNAKUMBUKA AHADI YAKO MARA

Na Robinson Wangaso, Musoma. 0765632944/ 0712735318

Imebaki miezi mitano tu, na siyo miaka mitano ufanyike uchaguzi mkuu bila kutekelezwa kwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwa wakazi wa mkoa wa Mara ya kukamilisha ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Mara lililopo katika eneo la Kwangwa manispaa ya Musoma kama alivyosema kwa miaka mitano Hospitali ya mkoa itakuwa imekamilika.


Akihutubia umati mkubwa katika mkutano hadhara wa kampeini mwezi Oktoba 2005 uliyohudhuriwa na wananchi wa mkoa huu kutoka wilaya zote rais Kikwete akiwa mgombea Urais kwa Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM aliahidi kuwa mkoa hauna hospitali yenye hadhi kutokana na uliyopo kuwa na majengo chakavu na haitoshi kutokana na ongezeko la wagonjwa kwani majengo ya hospitali hiyo yalijengwa zama za mkoloni.

" Mkoa wa Mara hauna hospitali yenye hadhi ya kimkoa, hii iliyopo imepitwa na wakati. Ni ahadi yangu kwenu kwa kipindi cha miaka mitano Hospitali yenu mpya itakuwa inafanya kazi, hii ni ahadi yangu kwenu na kamwe hamtanisuta baada ya miaka mitano" alisema raisi Kikwete.

Miaka ya 1980 wananchi wa mkoa wa Mara wakiwemo wakulima ambao walikuwa wakikatwa shilingi tatu kwa kila kilo moja ya pamba ambayo ilikuwa ikiuzwa katika vyama vya ushirika kwa wakati huo walichangia kwa zaidi ya miaka mitano ujenzi wa hospitali mpya ya mkoa ambapo jengo lake halikukamilika na kuishi njiani kwa kile kinachodaiwa kuwa usimamizi na matumizi ya fedha hizo haukuwa mzuri.

Ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo ilifikia ghorofa Tatu na kuishi hapo umekuwa ni kero kubwa ya wakazi wa mkoa wa Mara kwa serikali ambayo ilishindwa kusimamia fedha hizo za wananchi na kuwachukulia hatua wale waliokuwa wamekabidhiwa dhamana ya kusimamia ujenzi kwa niaba ya wananchi ambapo jasho la wanyonge kupotea bure bila huruma.

Kutokana na hali hiyo kuonyesha wananchi kupunguza imani na serikali yao kwa kushindwa kutimiza na kukamilisha azma ya wananchi, viongozi mbalimbali wakiwemi wale wanaowania nafasi mbalimbali za kisiasa wakiwemo wajumbe wa Halmashauri kuu ya taifa ya Chama cha Mapinduzi CCM wamekuwa wakitumia kero hilo katika kampeni wakitoa ahadi ya kukamilisha ujenzi huo pindi wakichaguliwa kwa kuisukuma serikali na baada ya kuchaguliwa huishia mitini.

Kero hiyo pia alifikishiwa rais Kikwete na alichaguliwa kuwa rais aliporudi katika ziara yake ya Kwanza mkoani Mara mwezi Januari 2006 ya kushukuru wakazi wa mkoa wa Mara na wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa Augosti 9 hadi 14 2006 alisema Serikali imekubaliana Kanisa Katholiki kukamilisha ujenzi huo ambao gharama za ujenzi zitatolewa kwa ushirikiano baina ya serikali na Kanisa hilo huku usimamizi wa ujenzi utakuwa chini ya kanisa.

Katika hotuba hiyo ambayo aliitoa katika viwanja hivyo hivyo vya shule ya msingi Mukendo, rais alisema hospitali hiyo itakalimishwa ujenzi wake na kufunguliwa kama hospitali ya Rufaa ili kusongeza karibu huduma ya matibabu kwa wananchi wa mkoa wa Mara na mikoa mingine ya kanda ya ziwa ambayo hawana hoaspitali za Rufaa na kuahidi kupanuliwa iliyokuwa hospitali ya mkoa ya zamani.

Wananchi wameshuhudia upanuzi ukifanyika lakini bado wanahoji, nguvu zao na michango yao ambayo waliielekeza katika ujenzi wa hospitali ya Kwangwa na kuahidiwa na viongozi wa kisiasa wakiwemo wale wa kitaifa kuwa ingekamilika zimetupwa au tena katika chaguzi zijazo ahadi zitaendelea kutolewa ambapo ni zaidi ya miaka 20 jengo hilo ambalo inasadikika limejengwa kwa ustadi mkubwa bila kukamilika.

Akionekana ni mwenye Ari, Nguvu na Kasi ya kutekeleza ahadi hiyo, rais alirudi Musoma Mwezi Agosti 31 mwaka 2006 kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa askofu wa jimbo la Musoma Mhashamu Justin Tetemu Samba ambapo alirudia kauli yake mbele ya waamini wa kanisa hilo na wananchi walijitokeza katika mazishi hayo kuwa mazungumzo na makubaliano baina yake na Askafu yalikuwa yamekamilika na hivyo aliomba msimamizi wa jimbo atakaechaguliwa na kanisa aendeleze juhudi hizo bila kuchelewesha ili serikali itoe fedha na ujenzi huo uanze.

" Mkoa wa Mara umepoteza mtu muhimu sana katika huduma za kiroho na maendeleo ya kijamii, Serikali ilikuwa na mkakati wa kushirikiana nae katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa mkoani hapa" alisema Rais Kikwete wakati wa salamu zake wakati wa mazishi hayo.

Mwezi Agosti 27 hadi Sepemba 1 2007 waziri mkuu wa wakati huo Edward Lowassa ambae alifanya ziara ya kikazi mkoani Mara ambae alionyesha kwa kipindi cha uongozi wake kufuatilia masuala muhimu za mkoa wa Mara yakiwemo mapigano ya koo za kabila la wakurya Tarime alifanya ziara mkoani Mara na kutembelea jengo hilo la Hospitali ikiwa ni kutaka kutekeleza ahadi ya seriakali ambapo alielezwa na msimamizi wa jimbo wa wakati huo Padre Julius Ogola kuwa kanisa lipo katika mchakato wa kuanza ujenzi tatizo ni fedha kwani ujenzi huo unagharimu fedha nyingi na serikali isaidie isaidie upatikanaji wake ili kazi ianze na waziri mkuu huyo aliahidi kuchukua hatua kwa haraka kwa ahadi hiyo ya serikali ya awamu ya nne kwa wananchi wa mkoa wa Mara.

Lowassa kaondoka madarakani, lakini najua waziri mkuu yupo na ofisi ya rais bado ipo? Je ni ninakila sababu ya kujihoji tatizo lipo wapi? serikali imesahaua ahadi zake au imedhamilia rais ili akutwe na wananchi wa mkoa wa Mara ambao ni wa wazi na wakweli wasio na soni hata kidogo baada ya miaka mitano ya serikali ya awamu ya nne kumalizika.

Wakati wa askofu mpya wa kanisa hilo Mhashamu askofu Michael Msongazila ulioyofanyika katika kanisa kuu la Maria mama wa Mungu, Lowassa alihudhuria sherehe hizo na kumshika mkono Mara baada ya kusimikwa rasmi na kumhakikishi kuwa serikali itashirikiana naye katika ujenzi wa hospitali ya rufaa. Lowassa aliondoka na serikali?


Hivi ni kweli ahadi hiyo haina kumbukumbu au kuondoka kwa Lowassa hakuna tena kiongozi wa serikali tofauti na rais kufuatilia ahadi alizotoa rais wakati wa kampeni ili zitekelezwe. Tunajua kuwa rais anazo shughuli na majukumu mengi, ndiyo maana wapo mawaziri, wakuu wa mikoa na ha wilaya ili kumsaidia kazi kutokana ma mfumo na mgawanyo wa madaraka ikiwa ni pamoja na kumkumbusha katika maeneo yao nini kinaendelea.

Kama ndiyo kwani ahadi siyo jambo muhimu kwa mkuu wa mkoa kumkumbusha rais, au tunasubiri kumpatia taarifa za matukio ya mauaji na mambo mengine huku ahadi hizo zikiwa zinakumbukwa vizuri na wananchi na wanasubiri wakati wa kampeni wamuulize "mzee ilituahaidi, ulisema kamwe hatutakuja kukusuta" ? Je rais utajibu vipi hapo?

Natumaini majukumu muhimu ya viongozi serikali katika mikoa ni pamoja na kujua wananchi wan shida gani na kipi wanamdai kiongozi wao wa kitaifa ndiyo maana ya uwakilishi na siyo kueleza mazuri tu kuwa unakubgalika mzee, je kwa nini msimwambie kuwa wananchi wanamdai nini ili watimizie.

Rais aliona umuhimu huo wa kuwa na hospitali ya mkoa ambao ni dhahili kila mmoja wetu anaukubali kutokana na huduma ya afya katika mkoa wa Mara kuwa inahitaji kupewa msukumo wa pekee kutokana na mkoa wenye wilaya sita unayo hospitali moja tu ya wilaya katika wilaya ya Tarime, huku wilaya ya Bunda wakitumia hospitali teule DDH inayomilikiwa na kanisa la KKKT, Wilaya ya Serengeti na Rorya hospitali zilizopo zinamilikiwa na kanisa la Menonite, Musoma vijijini na mjini hakuna hospitali ya wilaya na zinategemea hospitali ya mkoa.

,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,mwisho,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

1 comment:

  1. Ni kweli mkoa wetu lazima upate hospitali kubwa yenye kukidhi mahitaji ya wananchi..

    ReplyDelete